Wednesday, July 12, 2017

Mfahamu "Ebitoke" msanii wa komedi anayevuma kwa kasi Bongo Movie.

Komediani wa kike Bongo, Anastazia Exavery ‘Ebitoke’  anayefanya vizuri zaidi kupitia mitandao ya kijamii alipitia mambo mengi ikiwemo kufanya kazi za ndani ‘house girl’ huku dada yake akiwa kikwazo cha yeye kutoboa kisanaa. Hii ni historia yake aliyoitoa mwenyewe alipokuwa akihojiwa na kituo kimoja cha habari.
Maisha yake.
Ebitoke anafunguka: “Mimi ni Mkerewe ila nimezaliwa Kijiji cha Kiuwani Wilaya ya MulebaVijijini mkoani Kagera.
Elimu yake.
“Nilianza darasa la kwanza mwaka 2006 ambapo nilimaliza darasa la saba mwaka 2013 katika Shule ya Msingi Kalema iliyoko Chato mkoani Geita. Baada ya kumaliza shule ya msingi sikufanikiwa kuendelea na masomo hivyo nikajikuta nikiwa sina hili wala lile pale kijijini kwetu.
Ugumu wa maisha ulivyomzidia.
“Nilipoona maisha yanazidi kuwa magumu pale kijijini, nilikimbilia jijini Mwanza kwa ajili ya kutafuta kazi za ndani, nilifanikiwa kupata kazi nikiwa na dada yangu.
Baada ya kufika Dar.
“Nilifanya kazi zile za ndani kwa muda, baadaye mjomba wangu ambaye anaishi MbeziBeach (Dar), aliniita Dar ili nimsaidie kulea watoto wake na huo ndiyo ukawa mwanzo wa kulijua Jiji la Dar nikiamini huko ndiko ndoto yangu ya kuwa mwigizaji ingetimia.
Aondoka kwa mjomba wake.
“Baada ya kuona siwezi kutimiza ndoto zangu za kuigiza nikiwa kwa mjomba, mwaka 2015, niliondoka kwa mjomba na kwenda kwa rafiki yangu mmoja kule Kibaha, Pwani.


Aanza kuwa Mama-Lishe.
“Kutokana na ugumu wa maisha, nilianza kufanya kazi kwenye mgahawa kama Mama-lishe ili niweze kujikimu na kuepuka vishawishi vya hapa na pale.
Akutana na tangazo lililobadilisha maisha yake.
“Nikiwa naperuzi kwenye mitandao ya kijamii, nilikutana na tangazo kuwa Kampuni ya Timamu African Media inahitaji wasanii. Nikaamua kuomba nafasi, nikaitwa kwenye usaili, nikapita.
Afanya vitimbi ili afukuzwe kazi kwa boss wake.
“Niliposhinda usaili, nikawa ninatakiwa niende mazoezini, lakini ikawa ni ngumu kwa bosi wangu kunikubalia. Niliamua kuliamsha dude kwa kusudi ili nifukuzwe. Nikawa nikipewa kazi na bosi ninakataa, hapo ndipo nikafuzwa. Nilifanya vile ili nipate sehemu ambayo inaweza kunipa nafasi ya kwenda kufanya mazoezi.
Afanya kazi Bar.
“Nilipoona dada yangu hapendi niigize, niliamua kuhamia kwa rafiki yangu mwingine maeneo ya Tegeta (Dar) niliyekuwa ninaigiza naye. Alinitafutia kazi ya baa ambayo ilikuwa hainibani kwani nilipata nafasi ya kwenda kufanya mazoezi.
Ashindwa kazi ya Bar.
“Nilifanya kazi ya baa kwa miezi mitatu, nikaacha kwa sababu wanaume wengi walikuwa wananisumbua halafu wenzangu karibu wote walikuwa wanakwenda kwa mabwana zao. Nikaona ninaweza kushawishika.
Kazi ya kuwapikia wajenzi (vibarua).
“Niliondoka pale na kwenda kukaa kwa dada yangu kwenye nyumba nyingine ya mjomba. Nikapata kibarua cha kuwa ninawapikia wajenzi halafu wananilipa shilingi elfu tano kwa siku. Ilikuwa ni kazi ngumu sana kupika ugali wa watu 12.
Usaili uliobadilisha maisha yake.
“Baadaye Timamu Media walifanya usaili wa mtu ambaye anaweza kuigiza kishamba, nikafanikiwa kupita, kila mtu akasema ninaiweza vizuri nafasi hiyo.
Asili ya jina la "Ebitoke".
“Nikiwa mazoezini bosi wangu wa Timamu African Media, Timoth Kachumia aliniona ninavyocheza, ikabidi anipe jina la Ebitoke.

Mashabiki wampokea.
“Kilichonifanya niendelee kuipenda sini (kipande cha kuigiza) ya ushamba ni vile mashabiki walivyonipokea na kunikubali.
Mafanikio aliyoyapata.
“Sijapata mafanikio makubwa kihivyo kwa sababu ndiyo nimeanza, ila ninaweza kujihudumia baadhi ya vitu na nimefahamika. Mashabiki wangu wategemee mambo mazuri kutoka kwangu na kama kuna wadau na makampuni wanakaribishwa".
Share:

0 comments:

Post a Comment

Breaking News

Contact Us

Name

Email *

Message *

Translate

Total Pageviews